Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunaweza kufikia MDGs kuhusu afya katika siku 700: Ray Chambers

Tunaweza kufikia MDGs kuhusu afya katika siku 700: Ray Chambers

Wadau wanaopigia debe kufikia malengo ya maendeleo ya milenia kuhusu afya, wamewasilisha leo mkakati wa siku 700 wa kuwaokoa watoto milioni 2.2 kutokana na kifo, na hivyo kulifikia lengo la maendeleo ya milenia kuhusu afya ya mtoto ifikapo tarehe ya ukomo wake ya Disemba 31, mwaka 2015.

Mkakati huo unaunga mkono mkakati wa Katibu Mkuu Ban Ki-Moon wa ‘Kila Mwanamke, Kila Mtoto’, ambao unachagiza na kutoa msukumo wa kuboresha afya ya akina mama na watoto kote duniani, kwa kushirikiana na viongozi kutoka serikalini, mashirika mseto, sekta ya kibinafsi na sekta ya umma.

Katika taarifa ilotolewa wakati wa kongamano la kimataifa kuhusu uchumi, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu ufadhili wa malengo ya maendeleo ya milenia kuhusu afya na malaria, Ray Chambers amesema kuwa wakati zimesalia takriban siku 700 kabla ya tarehe ya ukomo wa malengo ya maendeleo ya milenia (MDGs), bado kuna fursa ya kuyafikia malengo hayo.

Bwana Chambers amesema ili kufikia lengo la milenia namba 4, idadi ya watoto wanaokufa wakiwa na umri wa chini ya miaka mitano itatakiwa kupunguzwa kutoka milioni 6.6 had chini ya milioni 4.3.