Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lamulika hali Mali, Darfur na Sudan Kusini

Baraza la Usalama lamulika hali Mali, Darfur na Sudan Kusini

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo, limekutana kufanya mashauriano kuhusu hali nchini Mali, pamoja na kujadili hali katika eneo la Darfur, Sudan na hali nchini Sudan Kusini. Joshua Mmali na taarifa kamili.

(TAARIFA YA JOSHUA)

Baada ya kuridhia taarifa ya rais wa Baraza hilo kuhusu hali nchini Mali, wanachama wake wamemsikiliza Msaidizi wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Operesheni za Ulinzi wa Amani, Herve Ladsous, ambaye amesema hali ya usalama Darfur imeendelea kuwa mbaya, na wakati mzozo wa Sudan Kusini ukichangia wakimbizi kumiminika mashariki mwa eneo hilo, na athari nyinginezo.

“Makundi yenye silaha Darfur yameripotiwa kushiriki katika mapigano ya Sudan Kusini. Jamii za wafugaji haziwezi tena kwenda Sudan Kusini kutafuta malisho msimu huu. Ningependa kusema kuwa mzozo huu unaweza kuvutia makundi mengi ya waasi Sudan, na hivyo kukanganisha juhudi za kupata suluhu, sio tu kwa mzozo wa Darfur, lakini pia mizozo ya majimbo ya Kordofan Kusini na Blue State, na pia kwa upana, juhudi za kuboresha uhusiano kati ya Sudan na Sudan Kusini”

Bwana Ladsous ameongeza kuwa mahitaji ya ulinzi wa raia katika eneo la Darfur bado ni mengi. Amesema juhudi ni lazima ziendelee kufanywa, ili kukabiliana na changamoto wanazokumbana nazo wahudumu wa kibinadamu na wanaotoa ulinzi, zikiwemo kuongeza msaada kwa UNAMID na juhudi za upatanishi.

Hata hivyo, amesema kupata suluhu la kudumu kunapatikana katika muktadha wa kisiasa, na hivyo, katika haja ya kusitisha mapigano na kufanya makubaliano ya kina.