Raia wa Uingereza afukuzwa Uganda; Kisa mapenzi ya Jinsia moja

23 Januari 2014

Takribani mwezi mmoja baada ya Ofisi ya Haki ya Umoja wa Mataifa kueleza hofu yake juu ya kupitishwa kwa sheria inayopinga mapenzi ya jinsia moja nchini Uganda, raia wa Uingereza, Bernard Randell amefukuzwa nchini humo baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika kwenye mapenzi hayo. Tayari Randell ameagizwa kuondoka nchini humo katika saa kumi na mbili, kama anavyo ripoti John Kibego wa redio washirika ya Spice FM nchini Uganda.

(Tarifa ya John Kibego)

Raia huyo wa Uingereza mwenye umri wa miaka 65, alikamatwa tarehe 25 Septemba mwaka jana pamoja na raia wa Uganda wakiwa na video ya mapenzi ya jinsia moja. Shitaka hilo lilitupiiliwa mbali na mkuu wa mashitaka ya umma, na baadaye kufufuliwa na mahakama kwa misingi kwamba kulipatikana ushahidi kuwa Randell aliendelea kuhusika na mapenzi hayo.

Akitoa uamuzi huo Hakimu Hellen Ajio alisema vitendo vyake vyakupotosha maadili haviwezi vumiliwa, na kuagiza aondoke katika kipindi cha saa 12 kwanzia dakika ya uamuzi.

Uamuzi huo umekuja wakati ambapo rais Yoweri Museveni amekataa kutia saini muswada wa kupinga mapenzi ya jinsia moja wa mwaka 2009.

Tarehe 28 Disemba mwaka jan, Rais Museveni aliurudisha bungeni, yeye akipinga adhabu ya maisha jela kwa wapenzi hao.

Aliwataja wapenzi wa jinsia moja kama watu wenye matatizo ya kiakili ambao wanahitaji kusaidiwa badala ya kuadhibiwa vikali.