Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Darfur changamoto ni nyingi lakini hatukati tamaa: Mkuu UNAMID

Darfur changamoto ni nyingi lakini hatukati tamaa: Mkuu UNAMID

Mkuu wa ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika kwenye jimbo la Darfur, UNAMID nchini Sudan Mohamed Ibn Chambas amezungumza na waandishi wa habari huko Khartoum akisema mwaka jana umeshuhudia ghasia zikishika kasi kwenye eneo hilo lakini ofisi yake haitokata tamaa ili kuendelea kuweka ulinzi na mustakhbali wa wakazi wa eneo hilo. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Ikiwa ni mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari tangu ashike wadhifa huo, Ibn Chambas amesema wamepata mafanikio ikiwemo vikundi zaidi kujiunga na makubaliano ya amani ya Doha licha ya kukumbana na changamoto kama vile mizozo ya kikabila, mapigano kati ya vikosi vya serikali na vile vyenye silaha, kuuawa kwa watendaji wa UNAMID, yote hayo yakiwa na madhara kwa raia. Amesema mwaka huu bado kuna changamoto hasa ya kushawishi vikundi zaidi vinasaini makubaliano yaDohahuku akituma ujumbe kwa wahusika..

(Sauti ya Chambas)

“Ujumbe wangu tangu mwanzo umekuwa bayana, baada ya miaka 10 ya mapigano, matumizi ya nguvu za kijeshi hayana nafasi na hayatatatua mzozo wa Darfur, na kukidhi mahitaji ya wananchi kwa dhati, yapaswa kuchagiza na kusongesha mbele njia pekee ya mazungumzo na mashauriano. Wakati amani na ulinzi ni muhimu, mahitaji halisi ya wananchi yanaweza kushughulikiwa kwa kuweka ajenda thabiti ya maendeleo ambayo itaboresha hali za kijamii na kiuchumi Darfur na kushawishi wanaoshi kambini au nchi jirani kurejea nyumbani.”

Bwana Chambas ameweka bayana kuwa UNAMID itaendelea kusimamia amani kwa mujibu wa mamlaka iliyopatiwa na itajilinda vyema pindi itakaposhambuliwa na kuendeleza ushirikiano na serikali ya Sudan hususan wizara ya Sheria.