Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa Montreux umekuwa wa mafanikio, sasa kazi kubwa inaanza Ijumaa: Ban

Mkutano wa Montreux umekuwa wa mafanikio, sasa kazi kubwa inaanza Ijumaa: Ban

Wakati wa kuchukua hatua za kijasiri ni sasa ili kumaliza madhila yanayokumba wananchi waSyria, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon huko Montreux, Uswisi baada ya mkutano wa ngazi ya juu wa kuonyesha mshikamano na Syria.

Bwana Ban amewaeleza waandishi wa habari kuwa mkutano huo ulikuwa wa mafanikio makubwa kwani kwa mara ya kwanza pande mbili pinzani zimekutana uso kwa uso na ameshukuru wajumbe kutoka pande 40 waliojitokeza kuonyesha mshikamano kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya amani kwa Syria siku ya Ijumaa huko Geneva.

Katibu Mkuu akasema…

(Sauti ya Ban)

 

“Wakati wa kuchukua hatua za uamuzi na za kijasiri ni sasa. Kazi ngumu zaidi inaanza Ijumaa, na jumuiya ya kimataifa imeonyesha mshikamano wao hii leo hapa inaunga mkono jitihada zinazohitajika Katika yote hapa tunapaswa kuweka katika fikra zetu matamanio ya raia wa Syria ya kuwa na amani na utulivu.”

Alipoulizwa kuhusu ugumu wa mazungumzo hayo hususan pande mbili kinzani kuwa mwenye meza moja na majaliwa ya siku ya Ijumaa, Bwana Ban amesema suala la msingi ni uaminifu na udhati wa kile mtu anachokisema.

Kuhusu hoja kwamba pande moja inataka suala la ugaidi lishughulikiwe huku nyingine ikiangazia zaidi chombo cha mpito, Katibu Mkuu amesema mwaliko wa mkutano ulihusu tamko la Genevala mwaka 2012 na akafafanua zaidi.

 (Sauti ya Ban)

“Kudhibiti  ugaidi ni muhimu sana. Nimejadili suala hili kwa kirefu na Waziri wa Mambo ya nje wa Syria. Lakini muhimu zaidi ni kuwa unapaswa kuwa na amani na utulivu na kuwapatia wananchi wote fursa ya kuendesha maisha yao na kuwapatia matumaini na hata hatma yao. Baada ya hapo magaidi na misimamo mikali  watapoteza mahali pa kuendelea kujitanua  kwani wamegawanayikwa kwa sababu wamekuwa wakipigana kwa zaidi ya miaka mitatu. 

Kuhusu sharti linalotakiwa na upande wa upinzani kuwa Rais Bashar Al Assad aondoke madarakani kama njia mojawapo ya kufanikisha mustakhbali wa Syria, Bwana Ban amesema..

(Sauti ya Ban)

 “Hilo ni  jambo linalopaswa kuamuliwa na wananchi wa Syria.Kwa hiyo hilo ni jambo linalopaswa kujadiliwa na pande mbili hizo chini  ya usuluhishi wa Lakhdar Brahimi.”