Surua yatishia uhai wa watoto nchini Guinea: UNICEF

22 Januari 2014

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF pamoja na wadau wake wameanza maandalizi ya kampeni ya kuwapatia chanjo dhidi ya Surua watoto zaidi ya Milioni Moja nukta Sita nchini Guinea ili kuepusha mlipuko wa ugonjwa huo hususan mji mkuu Conakry. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Mwakilishi wa UNICEF nchini humo Dokta Mohamed Avova amesema tangu mwezi Novemba mwaka jana kumekuwepo na wagonjwa 37 wa Surua mjini Conakry ambao wote ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 10 huku idadi hiyo ikiongezeka hivi karibuni na hata mtoto mmoja kufariki dunia.

Amesema hali hiyo imesababisha Wizara ya afya kutangaza rasmi mlipuko wa Surua mjini Conakry na viunga vyake na kwenye mikoa mingine. Dokta Avova amesema wana hofu juu ya hali hiyo na kwani ugonjwa huo unaambukiza kwa kasi hususan miongoni mwa watoto wadogo na wale wenye utapiamlo.

Amesema UNICEF itatoa chanjo, majokofu, sindano na vifaa vingine vya tiba na kampeni ya chanjo itaanza wiki chache zijazo pindi vifaa hivyo vitakapofikishwa maeneo husika. Halikadhalika UNICEF itaipatia serikali msaada kuwezesha tiba kwa wale walioambukizwa ugonjwa huo.