Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfumo mpya wa matumizi ya mazao ya baharini wahitajika: FAO

Mfumo mpya wa matumizi ya mazao ya baharini wahitajika: FAO

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO José Graziano da Silva amesema mabadiliko makubwa yanahitajika kufanyika kwenye matumizi ya mazao ya baharini ili kuweka uhakika wa chakula na ustawi wa maeneo ya pwani  na nchi za visiwani.

Akizungumza hukoAbu Dhabi, Bwana Da Silva amesema dunia haiwezi kuendelea kutumia rasilimali za bahari na maeneo mengine ya majini kama vile kamwe hazitoisha na haiwezekani kuendelea kutumia baharikamaeneo la kutupa taka.

Ameonya maeneo hayo sasa hivi yanakabiliwa na uchafuzi wa hali ya juu, uvuvi kupita kiasi na mabadiliko ya hali ya hewa na hivyo kutishia uwepo wao jambo ambalo amesema ni lazima liangaliwe upya.

Mkuu huyo wa FAO amesema mustakhbali wa sayari ya dunia yenyewe na hata afya ya wakazi wake na uhakika wa chakula, unategemea kiwango cha matumizi ya bahari.

Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 17 ya protini ya wanyama kwa binadamu inatokana na mazao ya baharini na kiwango ni kikubwa kwa nchi za visiwani. Hata hivyo asilimia 30 ya samaki duniani imevuliwa kupita kiasi na kusababisha hasara ya dola Bilioni 50 kwa mwaka.