Athari za usawa duniani ni kubwa kuliko ilivyodhaniwa: Profesa Stiglitz

20 Januari 2014

Kitisho cha kuendelea kuongezeka kwa ukosefu wa usawa duniani ni maudhui katika mjadala uliofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, mjadala ambao umeratibiwa na ubalozi wa Italia kwenye Umoja huo.

Hotuba maalum katika tukio hilo ilitolewa na mshindi wa tuzo ya uchumi ya Nobel kwa mwaka 2001, Profesa Joseph Stiglitz ambaye amesema mjadala huo umefanyika siku muafaka ambayo dunia inamkumbuka Martin Luther King Jr. mwanaharakati wa Marekani aliyetetea usawa. Amesema King alipinga siyo tu ubaguzi wa rangi bali pia ukosefu wa fursa sawa za kiuchum ikiwemo ajira, mambo ambayo yapo hadi leo.

Profesa Stiglitz amesema ukosefu wa usawa unagharimu nchi na hata dunia gharama kubwa kuliko ilivyodhaniwa hapo awali na wataalamu wa uchumi.

(Sauti ya Profesa Stiglitz)

Tunalipa gharama kubwa kutokana na ukosefu huu wa usawa. Tuna kiwango kidogo cha uchumi, kiwango kidogo cha utulivu, tunalipa gharama kidemokrasia na kugawa jamii. Jamii yenye mgawanyiko haifanyi kazi vizuri, haina mtangamano wa kutosha na kiwango kikubwa cha mizozo hususan kama msingi wa ukosefu wa usawa ni wa kijiografia au kikabila.”

Profesa huyo kutoka Chuo Kikuu cha Columbia akatupia lawama siasa na sera mbali mbali duniani ikiwemo zile za biashara kama vile sekta ya kilimo ambapo baadhi ya wakulima wanapatiwa ruzuku ilhali wengine wananyimwa.

(Sauti ya Profesa Stiglitz)

Kanuni za kimataifa zinahusika sana. Hii leo nchi nyingi kwa njia moja au nyingine zimekwama kutokana na kupindishwa kwa kanuni za kimataifa; biashara, uwekezaji, sekta ya fedha. Sote tumezingirwa na kanuni za kimataifa za fehda. Kwa hiyo kanuni za ushirikiano za kimataifa ni muhimu. Na jinsi kanuni za kitaifa zinavyosaidia kiwango cha usawa ndani ya nchi, vivyo hivyo hivyo kanuni za ushiriki za kimataifa zinabainisha kiwango cha usawa kati ya nchi na miongoni mwa nchi.