Ban avunjika moyo na hatua ya Iran kuhusu mazungumzo Uswisi; Sasa kufanyika bila Iran

20 Januari 2014

Siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kutangaza kuongeza idadi ya waalikwa ikiwemo Iran kwenye mkutano wa mashauriano kuhusu Syria huko Montreaux, Uswisi, hii leo amekaririwa akieleza kukatishwa tamaa na hatua ya Iran kubadili msimamo wa kile walichokubaliana.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Martin Nesirky amewaambia waandishi wa habari mjini New York kuwa baadhi ya waalikwa muhimu kwenye mazungumzo hayo yatakayofanyika Jumatano, wameweka masharti kuhusu kujumuishwa au kutojumuishwa kwa baadhi wajumbe. Miongoni mwa nchi hizo ni Iran, ambayo ilielezwa kukubali msingi wa mazungumzo hayo. Msingi wa mazungumzo hayo ya jumatano ni tamko la pamoja la Geneva la tarehe 30 Juni 2012 linalotaka kuundwa kwa maridhiano chombo cha mpito chenye mamlaka kamili ya utendaji.

(Sauti ya Martin)

"Katibu Mkuu amesikitishwa sana na taarifa zilizotolewa na Iran kwa wananchi hii leo ambazo haziendani na msimamo wake wa awali. Anaendelea kuisihi Iran kuungana na msimamo wa dunia juu ya tamko la pamoja la Geneva. Kwa kuzingatia kuwa Iran imechagua kuwa nje ya uelewa wa pamoja, Katibu Mkuu ameamua kuwa mkutano wa siku moja wa Montreaux utafanyika bila ushiriki wa Iran.”

Katibu Mkuu amesisitiza huu ni wakati wa kushinikiza harakati za amani Syria kwa misingi hiyo na kwamba huu si wakati wa kuongeza masharti.