Baraza la haki za binadamu latangaza mtaalam huru kuhusu CAR

20 Januari 2014

Rais wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, leo amemtangaza Bi Marie-Thérèse Keita Bocoum wa Côte d’Ivoire kama Mwakilishi Huru kuhusu Jamhuri ya Afrika ya Kati, kufuatia azimio lililopitishwa kwa kauli moja bila kupiga kura. Mtaalam huyo huru atatakiwa kuzuru Jamhuri ya Afrika ya Kati mara moja, na kutoa maelezo kwa Baraza hilo kuhusu hali ya haki za binadamu nchini humo.

Katika azimio hilo, Baraza la Haki za Binadamu limeelezea kusikitishwa na kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama nchini Car, na matukio mengi ya ukiukwaji wa sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, hususan, katika mauaji kiholela, ukamataji watu, utesaji, ukatili wa kingono dhidi ya watoto na wanawake, usajili wa watoto vitani na msahambulizi dhidi ya raia.

Baraza hilo limelaani vikali vitendo hivyo vyote vya ukiukwaji wa haki za binadamu, na kutaka vikomeshwe mara moja. Pia limetoa woto kwa pande zote katika mzozo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kuwalinda raia, hususan wanawake na watoto, dhidi ya ukatili wa kingono, na kuzingatia wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya haki za binadamu.