WFP inapungukiwa na chakula cha msaada CAR

20 Januari 2014

Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa mataifa WFP linapungukiwa na chakula cha kuwagawia idadi inayoongezeka ya wakimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. Shirika hilo linasema sababu kubwa ni hali ya usalama ambayo ni kikwazo kwa misafara iliyobeba chakula.

Malori 38 ya WFP yaliyobeba mchele yamezuiliwa kwenye mpaka wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na  Cameroon, sambamba na magari mengine 100. Kufuatia mapigano ya karibuni madereva wa malori ya biashara na yale ya WFP wamegoma kuvuka mpaka.

Athari zake kwa usambazaji wa chakula mji mkuu Bangui na maeneo mengine nchini humo ni maafa. Akiba ya nafaka ya WFP karibu inakwisha na kunde pia karibu zinamalizika.

WFP inasema kusitisha ugawaji wa chakula kunaweza kusababisha mvutano zaidi hususani miongoni mwa wakimbizi wa ndani 100,000 walioko katika kambi yenye msongamano mkubwa kwenye uwanja wa ndege wa Bangui.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa WFP wa kikanda Denise Brown amesema kama suluhisho la mwisho WFP inafikiria kusafirisha chakula kwa njia ya anga kutoka Douala, Cameroon, hadi Bangui., lakini kulazimika kuanzisha operesheni hiyo kutaongeza gharama kubwa kwa operesheni zao za dharura nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.