Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili hali Mashariki ya Kati na suala la Palestina

Baraza la Usalama lajadili hali Mashariki ya Kati na suala la Palestina

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limekutana leo kujadili hali ya Mashariki ya Kati, likiwemo suala la Palestina. Joshua Mmali ameufuatilia mkutano huo

Mkutano huo uliorodhesha wazungumzaji 47, umeanza kwa hotuba ya Katibu Mkuu, Ban Ki-moon, ambaye ameanza kwa kutoa wito kwa wote wanaohusika katika kongamano kuhusu Syria nchini Uswisi, kutilia maanani mahitaji ya watu wa Syria. Ban ambaye amekuwa ziarani Mashariki ya Kati siku chache zilizopita, amesema Iraq inakabikiliwa na tishio kubwa kwa utulivu wake

 “Nilijadilia hofu yangu na viongozi wengi wa Iraq na kuzisihi pande zote kuendeleza mazungumzo ya kisiasa, na kuzingatia utawala wa sheria na haki za binadamu. Leo, narejelea ujumbe wangu kwa viongozi wa Iraq kutimiza wajibu wao, kuhakikisha mazungumzo jumuishi, utangamano wa kijamii, na maendeleo yakinifu ya kisiasa.”

Kuhusu harakati za amani kati ya Israel na Palestina, Ban amesema viongozi wa Israel na Palestina watahitajika kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya amani.

“Ni lazima wawaandae watu wao kwa hatua hizi muhimu. Kushindwa kuendeleza hatua za suluhu la kisiasa kunaweza kuchochea kuzorota kwa hali zaidi. Nimesikitishwa na machafuko ya kila wakati na uchochezi kutoka pande zote, pamoja na kuendeleza vitendo vya kujenga makazi ambayo ni kinyume na sheria ya kimataifa. Kujenga makazi hakuendi sambamba na kujenga makubaliano ya amani ya kudumu.”