Juhudi zifanywe kuepusha mauaji ya kimbari CAR: Adama Dieng

20 Januari 2014

Mtaalam Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari, Adama Dieng, amesema hatua za dharura zinatakiwa kuchukuliwa ili kuepusha janga la mauaji ya kimbari katika Jahmhuri ya Afrika ya Kati.

Bwana Dieng ambaye amekuwa katika CAR hivi karibuni, amesema katika mahojiano ya Redio ya UM kuwa ingawa mzozo uliopo sasa nchini humo siyo wa kidini, kuna watu ambao wanajaribu kutumia dini ili kufikia malengo yao ya kisiasa.

Amesema mzozo huo unatakiwa kutafutiwa suluhu la kisiasa kupitia mazungumzo ya amani. Amesema juhudi zilizofanywa kufikia sasa zinatakiwa kuongezwa maradufu.

Tunatakiwa kuunga mkono ujumbe wa MISCA, ulio chini ya Muungano wa Afrika, AU, lakini pia ni muhimu kwamba askari wa Umoja wa Mataifa wapelekwe huko haraka iwezekananyo, ili tuhakikishe kuwa hali ya usalama siyo tu inarejeshwa, bali pia ili juhudi zifanywe kuwasaidia watu wa CAR kujenga taasisi mpya, kwani bila kuwepo utawala wa sheria na demokrasia, tutaona tena wimbi la machafuko katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.”