FAO yataja hatua muhimu za kupiga vita njaa na utapiamlo

17 Januari 2014

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limesema kuweka mifumo chakula ambayo inazingatia afya na endelevu ni mojawapo ya njia sahihi za kupiga vita njaa na  utapiamlo duniani.

Hayo yamesemwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO Helena  Semedo huko Berlin Ujerumani wakati wa mkutano wa imataifa wa chakula na kilimo kwa mwaka huu wa 2014. Amesema uzalishaji wa chakula umeongezeka mara tatu tangu mwaka 1945 na wastani wa kila mtu kupata chakula umeongezeka kwa asilimia 40. Hata hivyo amesema licha ya ongezekohilobado kuna kasoro kubwa jinsi ambavyo mifumo ya upatikanaji chakula inavyoendeshwa na hivyo lazima jitihada ziongezwe kurekebisha hali hiyo.

Amesema kasoro hizo zinasababisha jamii ya kimataifa kukumbwa na changamoto zitokanazo na lishe duni ambapo zaidi ya asilimia 50 ya wakazi wote Bilioni saba duniani wanakabiliwa na hali ya kutokuwa na chakula kabisa au kutumia chakula kwa kiasi cha kupindukia.

Mathalani watu Milioni 840 kila siku hawana chakula na hivyo kuathiri utendaji wao wa kazi na maendeleo ya jamii hususan watoto. Bi. Semedo amesema kilimo cha sasa si endelevu na hivyo ni vyema kurekebisha mifumo hiyo ili uzalishaji uendane na mahitaji ya sasa huku ukizangatia mahitaji  ya vizazi vijavyo.