Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wetu ni silaha thabiti ya kukabiliana na majanga yanayoendelea: Ban

Umoja wetu ni silaha thabiti ya kukabiliana na majanga yanayoendelea: Ban

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limehutubiwa na Katibu Mkuu Ban Ki-Moon akiangazia zaidi hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Umoja huo kwenye mizozo ya Syria, Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati na ile ya demokrasia ya Congo, DRC ambapo ametaka viongozi kuweka kando maslahi ya kitaifa na badala yake kushirikiana kwa pamoja na kumaliza mizozo hiyo kwa maslahi ya dunia nzima.

Bwana Ban amesema shuhuda za mwaka uliopita kuhusu hatua za pamoja zilivyozaa matunda kama vile kupitisha mkataba wa kimataifa wa kudhibiti biashara ya silaha ni kiashiria tosha kuwa Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.

Amesema katika muktadha huo, suluhu ya majanga huko Syria, DR Congo, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan kusini ni mshikamano miongoni mwa jamii nzima ya kimataifa.

(Sauti ya Ban)

“Lakini bado nasikitishwa na vitendo visivyo na maadili na vya kutowajibika kutoka kwa watu wengi ambao ni wana ushawishi na wana wajibu. Majanga niliyozungumzia leo yamo kwenye nchi zilizojaliwa maliasili, raia wenye uwezo wa kufanya kazi, historia za kipekee na hata fursa za amani na ustawi. Viongozi wanapaswa kuchukua hatua sasa kufikia maendeleo kwa maslahi ya wananchi na dunia yetu. Sote tunapaswa kusaka lengo moja la kuwa na suluhisho la pamoja katika matatizo yetu. “

Katibu Mkuu ametaka kila mmoja kutumia mwaka huu wa 2014 kuleta mabadiliko kwani anaamini kila raia wa dunia hii ana uwezo na ujasiri wa kubadili mazingira yawe bora kwa maslahi ya wote.