Wajasiriamali Zimbabwe sasa kuuza bidhaa zao Ulaya kirahisi

16 Januari 2014

Wajasiriamali wa kati na wadogo (SMEs) nchini Zimbabwe huenda wakaanza kushuhudia bidhaa zao zikipata soko Ulaya kufuatia makubaliano ya ufadhili wa kifedha kati ya Umoja wa Ulaya (EU) na kituo cha kimataifa cha biashra (ITC) wa zaidi ya uero milioni mbili katika mpango wa kuimarisha mazingira ya kibiashara ya nchi hiyo.

Ufadhili huu unaosimamiwa na mpango wa maendeleo ya biashara na sekta binafsi (TPSDP) kwa ajili ya Zimbabwe uanatarajiwa kukuza mazingira rafiki kwa wauzaji nje bidhaa wa nchi hiyo kutoka hatua ya kuuza malighafi hadi kuwa wazalishaji wa bidhaa za kuongeza thamani ya ushindani katika masoko ya kimataifa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa TPSDP Arancha González, Zimbabwe ni tajiri wa rasilimali na ujuzi wa watu wake na hivyo jambo muhimu ni kutumia mitaji ya kijamii kugeuza rasilimali kuwa ongezeko la thamani na bidhaa za nje ili kuwa na uchumi imara na mustakabali mwema wa nchi hiyo na watu wake.

Kwa upande wake mkuu wa ujumbe wa EU nchini Zimbabwe Aldo Dell'Ariccia, amesema katika kuwezesha hatua hiyo viwango vya kuuza bidhaa kwenye nchi za jumuiya hiyo pamoja na ushuru umeondolewa hatua itakayosaidia wajasiriamali hao.