Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Brahimi asikitishwa na NCC kujitoa kwenye ujumbe wa upinzani

Brahimi asikitishwa na NCC kujitoa kwenye ujumbe wa upinzani

Mwakilishi maalum wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa nchi za kiarabu kwenye mzozo wa Syria, Lakhdar Brahimi ameeleza masikitiko yake kufuatia hatua ya kikundi cha National Coordination Committee, NCC kujitoa katika ujumbe wa upande wa upinzani utakaoshiriki mkutano wa kimataifa wa amani kuhusu Syria wiki ijayo huko Uswisi.

Ameelezea hayo wakati wa mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa NCC Dokta Hassan Abdel-Azim. Bwana Brahimi amesema anaheshimu uamuzi wao lakini anasikitika kwani mkutano huo ni fursa ya kujadili jinsi ya kumaliza mapigano yanayoendelea nchini mwao.

Amesema anatambua mchango wa NCC na wanachama wake katika kuunga mkono demokrasia, uhuru na utu wa wananchi wa Syria, akiongeza kuwa amewafahamu vyema wafuasi wawili wa chama hicho wakiwemo  Abdul Aziz al-Khair na Rajaa Al-Nasser.  Wawili hao walikamatwa katika mazingira tatanishi kwa nyakati tofauti.

Hata hivyo  Bwana Brahimi ameitakia mema NCC na kusema ana uhakika itaendelea kufanya kazi ili kurejesha amani na demokrasia nchini Syria.