Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban afanya mikutano na viongozi kadhaa pembezoni mwa kongamano la Kuwait

Ban afanya mikutano na viongozi kadhaa pembezoni mwa kongamano la Kuwait

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amekutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa Kuwait, wakiwemo mfalme wa Kuwait, Sheikh Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al Sabah, Waziri Mkuu Sheikh Jaber Mubarak Al-Hamad Al-Sabah, na Naibu Waziri Mkuu Sheikh Sabah Khaled Al-Hamd Al-Sabah, pembezoni mwa kongamano la pili la kutoa ahadi za ufadhili wa kibinadamu kwa ajili ya Syria. Katibu Mkuu amewashukuru kwa mchango na ukarimu wao katika kusaidia kupunguza madhila ya watu wa Syria.

Katika muktadha huo huo, Ban amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Lebanon, Najib Mikati, ambaye amemshukuru kwa ukarimu wa nchi yake ambayo imewapa hifadhi idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wa Syria. Wamejadili kuhusu usaidizi kwa nchi jirani za Syria, ambazo zimeathiriwa na mzozo wa Syria, na pia kuhusu mkutano ujao Geneva kuhusu Syria.

Bwana Ban amekutana pia na Waziri wa Mipango na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jordan, Ibrahim Saif, ambaye ametoa shukrani zake kuhusu kazi ya Umoja wa Mataifa nchini Jordan, na ushirikiano uliopo katika kuwasaidia wakmbizi wa Syria. Ban ameisifu Jordan kwa ukarimu wake kwa wakimbizi wa Syria, huku akiiomba iendelee kuweka mipaka yake wazi kwa wakimbizi.

Mwingine aliyekutana naye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry. Bwana Ban na Bwana Kerry wamejadili hali nchini Syria na mkutano unaotazamiwa kufanyika mjini Geneva wiki ijayo. Wamejadili pia hali nchini Sudan Kusini, na uungwaji mkono wa juhudi za serikali za IGAD. Hali nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati pia imemulikwa katika mkutano huo.

Bwana Ban pia amekutana na kufanya mazungumzo na rais wa Shirikisho la Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu, Sir Nicholas Young, na kusifu juhudi na ujasiri wa wahudumu wa kibinadamu, hususan wale wa Hilali Nyekundu ya Syria.