Niliyoshuhudia Sudan Kusini ni mambo ya kutisha: Šimonovic

15 Januari 2014

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa masuala ya haki za binadamu, Ivan Šimonovic ambaye yuko ziarani nchini Sudan Kusini, ametembelea Bentiu, mji mkuu wa   jimbo la Unity na kusema alichoshuhudia ni jambo la kusikitisha.

Akizungumza akiwa kwenye moja ya kambi za wakimbizi wa ndani kwenye ofisi za ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNMISS, Bwana Šimonovic amesema alichoshuhudia Bentiu, ni kielelezo cha hali  ya kutisha ambapo jamii mbli zimelengwa na pande mbili tofauti. Akazungumzia kile alichoshuhudia barabarani.

(Sauti ya Šimonovic)

"Ilikuwa ni hali ya kutisha kuona maiti zimetapakaa barabarani na hazijatolewa siku tano baada ya kuuawa kwa sababu jamaa zao walikuwa na hofu.”

Ndani ya kambi aliyotembelea jamii inajitahidi kuendelea na maisha ambapo alikuta wanawake wakiendelea na maandalizi ya mlo kwa familia zao huku askari wa kulinda amani wa Umoja wa mataifa wakiwa wameimarisha ulinzi.

Ziara  ya Bwana Šimonovic nchini Sudan Kusini itamalizika tarehe 17 mwezi huu na lengo ni kutathmini hali ya kibinadamu na athari za mapigano yanayoendelea.