Ban asikitishwa na sheria ya kupinga ndoa za jinsia moja Nigeria

15 Januari 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameungana na mkuu wa haki za binadamu katika umoja huo Navi Pillay katika kueleza kusikitishwa kwake na hatua ya serikali ya Nigeria kutia saini sheria ya kupinga ndoa za jinsia moja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya msemaji wa katibu mkuu leo mjini New York, Bwana  Ban amesisitiza kuwa kila mmoja ana haki ya kupata haki za kimsingi na kuishi maisha ya utu na yanayostahili bila kubaguliwa kama inavyoelezwa katika tamko la dunia la haki za binadamu na mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Ameonyesha hofu yake kuwa sheria hiyo yaweza kuchochea ghasia na chuki kwa kuzingatia taarifa kwamba polisi kaskazini mwa Nigeria wanaripotiwa kuwashika watu wanaoaminika na mamalaka kuwa mashoga na kusema inawezekana polisi wamewatesa. Pia ameungana na shirika la Umoja wa Mataifa na ukimwi , UNAIDS na mfuko wa kimataifa wa kupamabana na ukimwi na kifua kikuu, Global Fund katika tamko lao hapo jana ambapo walisema sheria hiyo inaweza kuhatarisha juhudi za kupambana na Ukimwi.

Katibu huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema anaamini kwamba sheria hii yaweza kupitiwa upya na kwamba UM uko tayari kuisadia Nigeria katika kujenga mjadala na kubadilisha suala hilo.

Sheria hiyo inaelezwa kuwa inaopanua wigo wa makosa , kuvunja haki za binadamu ikiwamo kifungio cha mika 14 jela ikiwa watu wa jinsia moja watapatikana wakiishi pamoja au kujaribu kufunga ndoa  kwa karamu.