Kongamano la kimataifa lamulika uzuiaji wa uhalifu wa mauaji ya kimbari

15 Januari 2014

Leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa hapa New York limefanyika kongamano la kimataifa kuhusu uelewa wa tahadhari za mapema kuhusu mauaji ya halaiki, ikiwa ni miaka ishiri imepita tangu kufanyika mauaji ya kimbari nchini Rwanda. Joshua Mmali amefuatilia mazungumzo katika kongamano hilo

TAARIFA YA JOSHUA

Kongamano hilo lenye kauli mbiu: “mauaji ya kimbari ni uhalifu unaoweza kuzuiwa,” limeandaliwa na ubalozi wa kudumu wa Rwanda kwenye Umoja wa Mataifa na Kituo cha Kimataifa cha Wajibu wa Kulinda. Hotuba baada ya hotuba imeweka dhahiri jinsi kuitikia tahadhari inayotolewa mapema kunaweza kuzuia uhalifu wa mauaji ya kimbari. Wa kwanza kuzungumza amekuwa ni Balozi wa Rwanda nchini Marekani, Balozi Mathilde Mukantabana…

“Ni muhimu kukubali kuwa, uhai wa zaidi ya watu milioni moja ungeokolewa, ikiwa jamii ya kimataifa ingechukuwa hatua kufuatia onyo la mapema, hasa maelezo ya kina kuhusu mauaji ya kimbari yalopokelewa tarehe 11 Januari 1994. Hadithi za manusuru zitupe msukumo kutafakari na kuamua ikiwa tumekuwa wanafunzi wazuri wa janga hilo la historia.”

Baada ya Balozi Mukantabana, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson

“Tukiri kuwa mafunzo tuliyopata kwa miaka ilopita hayajafuatiwa na vitendo wakati wote. Tangu baa la Rwanda, mamia ya maelfu ya watu wameuawa kwa mauaji ya halaiki na makumi ya mamilioni kulazimika kuhama. Katika wiki chache zilizopita pekee, wanaume, wanawake na watoto wamechinjwa, siyo tu Sudan Kusini, bali pia katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, na katika jinamizi la Syria. Haya yote yanatokea kwa sababu ya migawanyo kwa misingi ya kidini na kikabila ambayo tunashuhudia katika mataifa mengi.”

Hata hivyo, Bwana Eliasson amesema hatua zimepigwa kwa kiasi fulani, hasa ukizingatia kinachofanywa na Umoja wa Mataifa kuwalinda raia Sudan Kusini