Maendeleo Syria yana mkwamo, michango yahitajika hima: Ban

15 Januari 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amezungumza katika mkutano wa pili wa kuchangisha fedha kwa ajili ya misaada ya kiutu kwa watu wa Syria,  mkutano unaofanyika Kuwait ambapo Ban amesisitiza michango hiyo ni muhimu sasa kwa kuwa mzozo unaendelea na kusababaisha mkwamo wa kimaendeleo na uvunjifu wa haki za binadamu. Taarifa zaidi na Flora Nducha

(TAARIFA YA FLORA)

Katibu Mkuu Ban amesema mapigano yanayoendelea yanazidi kuathiri raia huku akieleza kusikitishwa kwake na namna pande zinazopigana zinavyotumia ukatili dhidi ya wanawake na wasichana kama mbinu ya kuharibu utu wa wapinzani. Kuhusu matumizi ya silaha za maangamizi Ban amesema dunia inapinga matumizi hayo yasijirudie tena Syria kwani kilichotokea nchini humo kilikuwa kibaya kabisa kwa karne ya 21. Na kisha akawashukuru wale waliotoa ahadi zao za kusaidia kuikwamua nchi hiyo.

Kwa upande wake mkuu wa ofisi Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kiutu OCHA Bi Valerie Amos amesema mgogoro nchini Syria pamoja na mambo mengine umesababisha mgawanyiko wa kijamii, ukosefu wa mahitaji muhimu ikiwamo chakula, pamoja na kukosa matumaini na hivyo akataka ahadi za fedha kulenga kunusuru raia zaidi ya milioni tisa wanaohitaji msaada wa kibinadamu.

Bi Amos amesema huduma muhimu za kijamii zimeharibiwa nchiniSyriaakitolea mfano wa theluthi mbili ya hospitali za uma amabazo zimeharibiwa huku magari ya kubeba wagonjwa yakiwa yameharibiwa.

Mkuu huyo wa OCHA amesema alifanya ziara nchini humo miaka miwili iliyopita ambao karibu watu milioni walihitaji msaada lakini sasa inasikitisha kusema zaidi ya watu milioni tisa wanahitaji msaada wa haraka ili wakwamuliwe katika madhila ya vita.