Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pillay aomba ushirikiano wa kikanda ili kuwatia mbaroni wahalifu watoro

Pillay aomba ushirikiano wa kikanda ili kuwatia mbaroni wahalifu watoro

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, ametoa wito kwa viongozi wanaokutana katika mkutano wa ukanda wa Maziwa Makuu, ICGLR, wahakikishe kuwa watu wanaoshukiwa kutekeleza uhalifu wa kimataifa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu hawaendelei kukwepa mkono wa sheria kwa kuvuka mipaka na kukimbilia nchi jirani.

Bi Pillay amesema mkutano huo wa ngazi ya juu kuhusu ukanda wa Maziwa Makuu unaofanyika mjini Luanda, Angola, unatoa fursa maalum kwa nchi wanachama kuendeleza vita dhidi ya kutowajibika kwa watu wanaotenda uhalifu katika ukanda huo wenye ghasia za mara kwa mara.

Bi Pillay pia amesema malengo ya mkutano huo wa tano wa ICGLR, ni kuendeleza amani, usalama, utulivu na maendeleo, hna kwamba yanaweza kufikiwa tu ikiwa wale wanaoeneza ukatili na uhalifu wa kiuchumi wanawajibishwa.

Ametoa mfano wa Uganda na Rwanda, ambazo zimewapa hifadhi maafisa kutoka kundi la M23, ambao wanadaiwa kutekeleza ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, ukiwemo ubakaji, mauaji ya halaiki, usajili wa watoto jeshini, akisema kuwa ikiwa wataendelea kukwepa sheria kwa kuwa katika nchi jirani, watabaki kuwa tishio kwa usalama na hivyo kuzuia juhudi za amani na maendeleo endelevu kwenye ukanda huo.