Afisa wa haki za binadamu kuzuru Sudan Kusini:

14 Januari 2014

Msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu haki za binadamu Ivan Šimonović, anazuru Sudan Kusini kuanzia leo htarehe 14 Januari hadi tarehe 17 Januari ili kutathimini hali ya haki za binadamu nchini humo, athari za mapigano ya karibuni na kubaini maeneo ya kuboresha hasa pale ambapo raia wameathirika.

Katika ziara yake ya siku nne Šimonović akiwa Juba atakutana na maafisa wa serikali, tume ya kitaifa ya haki za binadamu, wanadiplomasia na jumuiya za kijamii wakiwemo viongozi wa  kijamii na kijadi.  Pia atatembelea wakimbizi wa ndani, waathirika na wafungwa mjini Juba.

Ana mipango ya kusafiri kuelekea Malakal, Bentiu  na  Bor, mji uliopo kilometa 200 kaskazini mwa Juba ambako kumekuwa na mapigano makubwa hivi karibuni.

Katika taarifa yake ya karibuni kamishina mkuu wa haki za binadamu Navi Pillay ameelezea hofu kubwa kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu, na usalama wa wale wanaokamatwa,, wakiwemo mamia ya raia walioripotiwa kuwekwa rumande wakati wa msako wa nyumba hadi nyumba.