IOM yaanza kurejesha nyumbani raia wa Mali kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati

14 Januari 2014

Shirika la kimataifa la uhamiaji, IOM linaanza kusafirisha kwa ndege takribani wahamiaji 550 wa Mali waliokuwa wanaishi Jamhuri ya Afrika ya Kati na hiyo ni kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo na kutishia maishayao. Mpango huo unafuatia ombi la serikali yaMaliambapo ndege mbili zitaanzia safari Bangui hadi mji mkuu wa Mali,Bamako.

Msafara huo unakuja baada ya IOM kukodisha ndege tatu kwa ajili ya kuwarejesha nyumbani wahamiaji kutokaChad. Tangu kuanza kwa mapigano zaidi ya wahamiaji Elfu Sitini wameomba ofisi za ubalozi wao nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kuwasaidia kurejea nyumbani kutokana na mapigano ambapo IOM inasema hadi sasa raia Elfu 33 bado wanahitaji huduma hiyo.

Mkuu wa IOM nchini Mali Bakary Doumbia anasema wengi wanaorejea wamekumbwa na kiwewe kutokana na ghasia walizoshuhudia na hivyo watahitaji usaidizi zaidi ili waweze kutangamana ndani ya jamii zao.

Tayari IOM imezindua ombi la dola Milioni 17.5 ambapo dola Milioni 10 kati ya hizo zitasaidia kuwasafirisha kwa njia ya ndege wahamiaji ilhali kiasi kinachobakia kitasaidia utangamano kwenye nchi zao.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter