Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAIDS na Global Fund wahofia sheria mpya Nigeria kuathiri vita dhidi ya ukimwi:

UNAIDS na Global Fund wahofia sheria mpya Nigeria kuathiri vita dhidi ya ukimwi:

Shirika la Umoja wa Mataifa la linalohusika na ukimwi UNAIDS na fuko la kimataifa la kupambana na ukimwi, kifua kikuu na malaria Global Fund, wameelezea hofu yao dhidi ya fursa ya huduma kwa waathirika wa ukimwi ambao ni wasagaji, mashoga, wanaoshiriki mapenzi ya jinsia tofauti tofauti na waliobadili jinsia (LGBT), kwamba itaathirika pakubwa kutokana na sheria mpya nchini Nigeria inayoharamisha na kufanya kuwa kosa la jinai watu wa aina hiyo, mashirika na shughuli zao na watu wanaowaunga mkono. Joseph Msami na maelezo kamili

(TAARIFA YA JOSEPH MSAMI)

Sheria hiyo mpya huenda ikazuia fursa ya huduma muhimu za HIV kwa watu wa LGBT ambao wako katika hatari ya kupata maambukizi ya HIV, na hivyo kudhoofisha mafanikio ya mipango ya Rais kwa ajili ya HIV/AIDS iliyozinduliwa miezi kadhaa iliyopita na Rais Goodluck Jonathan. Madhara ya sheria hiyo kwa afya, maendeleo na haki za binadamu ni ya mbali kuyafikia Nchini Nigeria mapenzi ya jinsia moja tayari ni kosa la jinai kwa muda sasa, lakini sheria mpya imeongeza na makundi mengine yaundayo LGBT.

Sheria hiyo mpya inasema “ Mtu yoyote anayeandikisha, kuendesha au kushiriki clubs za mashoga, jumuiya na mashirika yao, moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, kudhihirisha hadharani uhusiano wa kimapenzi wa jinsia moja nchini Nigeria atakuwa anafanya kosa la jinai na anaweza kushitakiwa na kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 jela.