Ban atembelea wakimbizi wa Syria nchini Iraq

14 Januari 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameongoza ujumbe mzito kwenye kambi ya Kawrgosik,  eneo la Kurdistan nchini Iraq ambayo inahifadhi wakimbizi kutoka Syria, katika ziara hiyo aliambatana na Mkuu wa shirika la wakimbizi duniani, UNHCR. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya

(Taarifa ya Grace)

Bwana Ban ameshuhudia hali halisi kwenye kambi hiyo akisema amesikitishwa sana kuona wanawake na watoto wakitaabika na janga hilo la Syria linalosababishwa na binadamu. Amepata fursa ya kutembelea familia kwenye mahema, kuzungumza nao na kufahamu matarajio yao.

(Sauti ya Ban)

“Nilichoshuhudia kinakatisha tamaa. Nimekutana na familia ya wakimbizi kwenye hema yenye watoto wawili wa kike. Nimesikitishwa na machungu yao. Familia zinajitahidi kuendelea kuishi na kushirikiana kutafuta wapendwa wao waliopotea na hata kufarijiana wakati wa machungu ya kupoteza wapendwa wao. Familia hizi zilitaka maisha bora lakini sasa zinaishi kwa hofu na bila uhakika wa mustakhbali wao.”

Hata hivyo ameshukuru serikali ya mkoa ya Kurdistan kwa kuhifadhi wakimbizi Laki Mbili kutokaSyria. Bwana Ban amewataka wawe na imani na Umoja wa Mataifa kwani mkutano wa kesho kuhudu usaidizi wa kibinadamu na wa wiki ijayo Uswisi kuhusu amani nchini Syria unaonyesha nuru.