Makazi mapya kwa wakimbizi yaandaliwa, mji wa Bor washikilwia na waasi: UNMISS

13 Januari 2014

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS unaandaa eneo jipya la makazi kwa wakimbizi wa ndani kutokana na kuendelea kumiminika kwa raia wa nchi hiyo kunakosababishwa na mapigano  yanayoendelea katika baadhi ya maeneo nchini humo. Msemaji wa Umoja wa Mataifa Martin Nesirky amewaambia waandishi wa habari mjini New York kuwa hivi sasa UNMISS katika makazi yake  10 nchini Sudan Kusini inahifadhi wakimbizi wa ndani zaidi ya Elfu Sitini.

 (Sauti ya Martin)

“Ujumbe huo hivi sasa uko katika harakati za kuaandaa eneo  jipya kwa raia waliokimbia makazi yao huko Juba. Tayari kuna wakimbizi wa ndani Elfu Thelanini wanaosaka hifadhi kwenye ofisi za UNMISS zilizoko mji mkuu Juba.”

UNMISS imesema vikosi vya  upinzani vinadhibiti mji wa Bor, kwenye jimbo la Jonglei na kuna ripoti za mapigano ya hapa na pale karibu na ofisi zake huku hali ya utulivu ikiripotiwa huko Bentiu kwenye jimbo la Unity. Doria iliyofanywa na askari wa UNMISS kwenye eneo la Bentiu ilishuhudia uporaji na kuchomwa kwa makazi ya watu.