Mkakati wa amani, usalama na Ushirikiano bado ndio matumaini ya ukanda wa Maziwa Makuu: Bi Robinson

13 Januari 2014

Mwakilishi Maalum wa Katibu mkuu kuhusu ukanda wa Maziwa Makuu, Mary Robinson, ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo kuwa manthari ya matumaini yaloghubika hali mashariki mwa Kongo kufuatia kutia saini makubaliano yalotokana na mkutano ulioongozwa na rais Museveni wa Uganda na Rais Joyce Banda wa Malawi, sasa yametoweka, kwani ukanda wa Maziwa Makuu unapitia katika wimbi jingine la machafuko.

Amesema mbali na machafuko yalosababisha vifo vya zaidi ya watu 50 mashariki mwa DRC kwenye mji wa Kamango na watu wengine zaidi ya 100 kwenye miji mingine, katika mashambulizi kadhaa, hali katika Jamhuri ya Kati pia iliendelea kuzorota katika siku chache zilizopita, huku mapigano yakiibuka nchini Sudan Kusini.

Bi Robinson amesema, wakati tarehe ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu kusaini mkakati wa amani, usalama na ushirikiano ulotiwa saini mjini Addis Ababa, licha ya hali dhoofu kiusalama iliopo sasa, mkakati huo bado ndio unaotoa nafasi nzuri kabisa ya kuleta amani na utulivu katika ukanda wa Maziwa Makuu.

Robinson

Karibu mwaka mmoja tangu uliposainiwa, mkakati huo unaendelea kushikilia matumaini ya amani na utulivu katika ukanda. Hata hivyo, kilicho muhimu hata zaidi kwa hatua za kina, ni utekelezaji wa ahadi zote, kwenye ngazi za kitaifa na kikanda, ili kuleta matunda ya amani na kuboresha maisha ya watu kwenye ukanda kwa njia ya kudumu. Nawategemea nyie kama wanachama wa Baraza la Usalama kuendelea kuunga mkono mkakati huo, na kuwahimiza wahusika wote kutekeleza kikamilifu ahadi zao.”