Jamhuri ya Afrika ya Kati iko katika kipindi muhimu: Babacar Gaye

13 Januari 2014

Jamhuri ya Afrika ya Kati iko katika kipindi muhimu hivi sasa kitakachoamua hatma ya nchi hiyo, amesema mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika  ya Kati, Jenerali Babacar Gaye alipozungumza na waandishi wa habari mjini New York, kwa njia ya simu kutoka mji mkuu Bangui.

Amesema baada ya kujiuzulu kwa viongozi wa mpito wiki iliyopita na kutangazwa kwa mtendaji wa mamlaka ya mpito wa kusimamia maandalizi ya uchaguzi, jukumu la jamii ya kimataifa ni kusaidia mamlaka za mpito kufanikisha uchaguzi na kumaliza mateso yanayokumba wananchi kutokana na imani zao za kidini na hata muonekano wao.

 (Sauti ya Jenerali Gaye)

“Leo naweza kusema matumaini yanaweza kupatikana. Matumaini yako mikononi mwa kuimarishwa kwa kikosi cha Afrika, MISCA kinachosubiri askari wengine kutoka Rwanda. Matumaini yanategemea pia kuendelea kwa ushiriki wa SANGARI ambavyo ni vikosi kutoka Ufaransa na tunawashukuruku kwa kile walichofanya kwa ushirikiano na MISCA. Halikdhalika kwa kufanyika mapema uchaguzi wa Rais wa mpito. Sifa za mtendaji mpya wa mpito, zimesaidia kurejesha matumaini. Natumai kwamba uteuzi wa Waziri Mkuu na  wa serikali utaimarisha zaidi matumaini hayo.”

Kwa mujibu wa Jenerali Gaye janga la takwimu zinaweka bayana janga la Jamhuri ya Afrika ya Kati ambapo raia mmoja kati ya watano ni mkimbizi wa ndani na watu Laki Moja wamesaka hifadhi kwenye uwanja wa ndege mjini Bangui.