Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mitandao ya kijamii yaweza kujenga au kubomoa haki za mtoto: Pillay

Mitandao ya kijamii yaweza kujenga au kubomoa haki za mtoto: Pillay

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Navi Pillay amefungua mkutano wa kamati ya mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto, CRC huko Geneva, Uswisi na kusema kuwa mitandao ya kijamii inaweza kujenga au kubomoa haki za mtoto iwapo haitaangaziwa vyema.

Amesema kupitia mitandao hiyo, watoto na hata jamii wanaweza kupata taarifa mpya juu ya kulinda na kutetea haki za mtoto lakini bado kuna changamoto kubwa.

(Sauti ya Pillay)

“Hili ni eneo gumu. Ni kwa vipi tunaweza kutofautisha kati ya kumlinda mtoto dhidi ya taarifa potofu kwenye intaneti kwa kuzua au kuchuja taarifa na wakati huo huo kumjengea uwezo kupitia mitandao hiyo? Hii ni changamoto kubwa. Hivyo natiwa moyo na nawapongeza kwa uamuzi muafaka wa kutenga mjadala huu wa wazi wa mwaka 2014 kuangazia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na haki za mtoto.”

Mkataba wa haki za mtoto uliridhiwa mwaka 1989 na unatangaza haki kuu nne za msingi za mtoto ambazo ni Kuishi, kuendelezwa, kushirikishwa na kulindwa.