Mtaalamu wa UM aitaka serikali ya Kenya kulinda haki za wanaofurushwa Msitu wa Embobut

13 Januari 2014

Mtaalam huru wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa ameitaka serikali ya Kenya kulinda haki za watu wa jamii ya kiasili ya Sengwer, ambao wanaripotiwa kukabiliwa na hatari ya kufurushwa kutoka kwenye msitu wa Embobut kwenye milima ya Cherangani magharibi mwa Kenya.

Mtaalamu huyo kuhusu haki za watu wa asili, James Anaya amesema amesikitishwa na ripoti kuwa polisi wanapanga kuwafurusha watu hao wa jamii ya Sengwer kwa lazima, huku akitaka serikali ya Kenya ihakikishe viwango vya sheria ya kimataifa vinatimizwa katika kulinda haki za watu wa asili.

Akinukuu vipengee vya Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wa asili, Bwana Anaya amesema watu wa asili hawapaswi kuondolewa kwa lazima kwenye ardhi zao au maeneo wanayokaa, na kwamba hakuna shughuli yoyote ya kuwahamisha inayopaswa kutekelezwa bila hiari yao au bila kulipwa fidia inayofaa, pamoja na kupewa fursa ya kerejea kwenye maeneo hayo pale inapowezekana.