Ariel Sharon afariki dunia, Ban atuma rambirambi

11 Januari 2014

Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Ariel Sharon amefariki dunia leo ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametuma risala za rambirambi kwa serikali na wananchi wa Israel. Katika salamu hizo Bwana Ban amesema Sharon atakumbukwa kwa jinsi alivyojitoa wakati wa uhai wake kwa nchi yake na alikuwa shujaa kwa wananchi wake wakati akihudumu kama askari na pia kiongozi. Amesema Sharon atakumbukwa kwa ujasiri wake wa kisiasa na azma yake ya kusongesha mbele uamuzi wa kihistoria na wenye machungu wa kuondoa walowezi na vikosi vya Israel kutoka Ukanda wa Gaza. Katibu Mkuu amesema waliofuata baada ya yeye sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kutimiza matamanio ya amani kati ya Israel na Palestina. Bwana Ban ametaka Israel kuendeleza mchango wa hayati Sharon wa kusonga mbele bila hofu katika kuwa na TAifa la Palestina likiwepo salama na sambamba na TAifa la Israel.Amesema wakati huu wa majonzi, Umoja wa mataifa kwa upande wake unarejelea azma yake ya kushirikiana na serikali na wananchi wa Israel kwa ajili ya amani na usalama. Waziri Mkuu huyo wa zamain wa Israel alikuwa na umri wa miaka 85.