Baraza la Usalama lasema mzozo wa Sudan Kusini usiingiliwe na majeshi ya kigeni

10 Januari 2014

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa taarifa likisema mzozo wa Sudan Kusini hautakiwi kuingiliwa na nguvu za kijeshi za kigeni. Taarifa hiyo inafuatia mkutano wa Baraza hilo hapo jana, ambapo lilisikiliza ripoti za Mkuu wa Idara ya Operesheni za Ulinzi wa Amani, Hervé Ladsous, Mwakilishi wa Katibu Mkuu na Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS, Hilde Johnson na Mwakilishi wa Katibu Mkuu kuhusu Sudan na Sudan Kusini, Haile Menkerios kuhusu hali Sudan na Sudan Kusini.

Wanachama wa Baraza hilo walisisitiza uungaji mkono wao wa dhati kwa juhudi za upatanishi ambazo zinaongozwa na nchi wanachama wa IGAD, na kukaribisha kuteuliwa kwa timu ya upatanishi ya IGAD, ikiongozwa na Balozi Seyoum Mesfin wa Ethiopia, ambayo inatarajiwa kutafuta suluhu la amani kwa mzozo wa Sudan Kusini.

Wametilia msisitizo haja ya Rais Salvar Kiir, Makamu wake wa zamani, Riek Machar na viongozi wengine wa kisiasa kuonyesha busara yao katika uongozi kwa kuafikia mara moja usitishaji mapigano na kuanza mazungumzo ya kina kama ilivyopendekezwa katika juhudi za upatanishi za IGAD ambazo zinaendelea mjini Addis Ababa.