Mkutano wa kuchangisha fedha kwa ajili ya Syria ni muhimu zaidi sasa: OCHA

10 Januari 2014

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kiutu OCHA imesema mkutano wa pili wa kuchangisha fedha kwa ajili ya kuinusuru Syria utakaofanyika mjini Kuwait wiki ijayo ni muhimu hasa kwa kuzingatia kuwa hali ya kiutu nchini humo ni tete na inazidi kuzorota.

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva leo msemaji wa OCHA Jens Larke amesema zaidi ya watu milioni tisa nchini Syria wanahitaji msaada huku watu milioni sita na nusu wakiwa ni wakimbizi wa ndani. Larke amesema watu milioni mbili na laki tatu wamekimbilia nchi jirani na kaskazini mwa Afrika tangu Januari mwaka 2012 nusu yao wakiwa ni watoto.

Hapa mjini New York Katibu Mkuu wa Umoja wa Mafatia atakayeongoza mkutano huo amezitaka nchi washiriki katika mkutano huo kuja na mkakati wa kukomesha mapigano.

“Tunatarajia kwamba nchi zote zitakazoshiriki zitakuja na nia thabiti kusaidia mchakato huu kusonga katika muelekeo sahihi ili tushuhudie mwisho wa  machafuko haraka iwezekanavyo”

Mkutano huo utawaleta pamoja viongozi wa mataifa mbalimbali wanachama wa UM na vuiongozi wa mashirika mbalimbali ya umoja huo ikiwamo lile la wakimbizi UNHCR Litakalowakilishwa na mkuu wake Antonio Guterres, na Valerie Amos atawakilisha ofisi ya kuratibu misaaada ya kiutu, OCHA