Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamati ya IPU yakutana kushughulikia masuala ya haki za binadamu za wabunge

Kamati ya IPU yakutana kushughulikia masuala ya haki za binadamu za wabunge

Kesi kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu za wabunge 262 zitatathminiwa na Kamati ya Haki za Binadamu ya Muungano wa Wabunge Duniani, IPU, wakati itakapokutana wiki ijayo mjini Geneva.

Kamati hiyo ambayo itakutana kuanzia tarehe 13-17 Januari, pia itachunguza uwezekano wa kuwepo kesi nyingine zinazohusisha mauaji ya wabunge, kukamatwa kiholela na kubinywa kwa uhuru wa kujieleza wa wabunge nchini Iraq, Oman na Yemen.

Bara la Afrika ndilo lenye idadi kubwa zaidi ya wabunge wenye kesi zinazoshughulikiwa na kamati hiyo ya IPU, ikiwa na wabunge 113 walio na kesi, ikifuatiwa kwa karibu na Asia iliyo na wabunge 94. Kamati hiyo pia inashughulikia kesi zinazowahusisha wabunge 39 kutoka mabara ya Amerika na 16 kutoka Uropa.

Takriban wabunge 200 miongoni mwa wabunge hao ni kutoka kwa vyama vya upinzani, lakini wabunge 53 ambao haki zao zimekiukwa ni wa kutoka katika vyama tawala.