Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Senegal yakaribia kutokomeza mbun’go

Senegal yakaribia kutokomeza mbun’go

Mradi unaotekelezwa na shirika la kilimo na chakula duniani, FAO nchiniSenegalwenye lengo la kutokomeza mbung’o umeanza kuonyesha dalili ya kushinda vita dhidi ya wadudu hao hatari kwa mifugo.

Meneja mradi huo kutoka Wizara ya Mifugo Baba Sall amesema tangu kuanza kwa mradi mwaka 2012, idadi ya wadudu hao imepungua kwa kiasi kikubwa kwenye eneo la Niayes karibu na mji mkuu Dakar.

Amesema eneo hilo lina mazingira bora kwa mbung’o kuzaliana na hivyo kusababisha ugonjwa wa homa ya malale kwa mifugo hususan ng’ombe wa maziwa na wale wa nyama.

Sall amesema mradi huo unaotumia teknolojia ya kuzalisha madume tasa ya mbung’o ambayo yanapokutana na mbung’o jike hayawezi kupata watoto umepunguza idadi ya mbung’oporiwarukao kwa asilimia 99 ndani ya miezi Sita.

Amesema mbinu hiyo ni rafiki kwa mazingira kwani hakuna dawa inayotumika kwa wanyama kuwakinga na wadudu hao. Wadau wengine katika mradi huo ni pamoja na shirika la nishati ya atomiki la Umoja wa Mataifa, Marekani na Ufaransa.