Mashirika ya UM yazidi kutiwa hofu na usalama wa wakimbizi wa ndani Sudan Kusini

10 Januari 2014

Zaidi ya watu 231,000  wametawanywa na machafuko hadi sasa Sudan Kusini tangu yalipozuka Desemba 15 mwaka jana imesema ofisi ya Umoja wa mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA. Flora Nducha na taarifa kamili

(TAARIFA YA FLORA NDUCHA)

Kwa mujibu wa ofisi hiyo watu wengine 43,000 wamekimbilia mataifa jirani yaKenya,Uganda,SudannaEthiopia.

OCHA inasema takribani watu 60,500 wametafuta hifadhi katika vituo 10 vya Umoja wa Mataifa Sudan Kusini. Alhamisi mkuu wa OCHA  Valerie Amos ametangaza fungu la dola milioni15 lililotengwa ili kuwezesha kukidhi mahitaji ya kibinadamu Sudan Kusini kwa watu ambao wanahitaji haraka misaada ya malazi na usalama.

Mashirika ya Umoja wa mataifa yatatumia fedha hizo kuboresha hali ya maisha katika kambi za wakimbizi wa ndani ,kusafirisha watu wanaohitaji huduma za tiba na kusafirisha wahudumu wa afya katika maeneo ambayo hayafikiki au ni hatari saana kwa njia ya barabara.

Marixie Mercado msemaji wa shirika la Umoja wa mataifa la watoto anasema usalama na hali ya kina mama na watoto inatia wasiwasi  kwani wao ndio idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani

(SAUTI YA MARIXIE MERCADO)

 “Hali katika kambi za Juba ni mbaya saana , lakini UNICEF inahofia zaidi hususan hali ya kambi ambazo hatuwezi kuzifikia sababu ya mapigano. Wakimbizi wa ndani ambao wengi ni wanawake na watoto wanakabiliwa na uhaba wa chakula, maji na huduma za usafi. Hivi sasa kuna visa saba vya surua kwenye kambi za Juba, na vingine vitatu katika kambi ya Bentiu .UNICEF inashirikiana na wadau wengine kuwafikishia wakimbizi wa ndani huduma ya dharura ya maji, usafi, maliwato na huduma za lishe. Katika kampeni ya chanjo pamoja na wizara ya afya , WHO na qwadau wengine imewafikia watoto 30,000 walio chini ya umri wa miaka 15 katika kambi za Juba. Chanjo hizo ni za surua, polio, vitamini A na dawa za kuua minyoo. Sasa tunawalenga watoto wengine 37,000 kwa ajili ya chanjo katika kambi za Awerial na Bentiu.”

Umoja wa mataifa umeomba dola milioni 166 iki kuweza kutoa msaada kwa wakimbizi wa ndani Sudan Kusini kati ya Januari na Machi