Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwelekeo wa kuimarisha kikosi cha UNMISS ni mzuri: Ladsous

Mwelekeo wa kuimarisha kikosi cha UNMISS ni mzuri: Ladsous

Mwelekeo wa kutekeleza azimio la Baraza la Usalama kuhusu kuimarisha kikosi chake cha ulinzi wa amani Sudan Kusini, UNMISS uko sawa licha ya shaka zinazodaiwa kuwa zilijitokeza.

Amesema Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani ndani ya Umoja wa Mataifa Hervé Ladsous alipozungumza na waandishi wa habari mara baada ya mashauriano ya faragha ya baraza la usalama kuhusu Sudan Kusini. Katika mazungumzo hayo alieleza kuwa baadhi ya polisi wameshawasili na kundi lingine wanatarajiwa wiki chache zijazo. Hata hivyo aliulizwa kuhusu madai ya kwamba baadhi ya askari hawakubaliwi..

(Sauti ya Ladsous)

Awali kulikuwa na baadhi ya maoni ambayo yalitia shaka, walikuwa wanahoji kuwa askari kutoka baadhi ya nchi fulani hawakubaliki, hili lilitutia shaka. Lakini hali sasa imekuwa bora kwa maana kwamba ujumbe umekuwa wazi. Lakini sasa tuko katika nafasi ya kupeleka askari ambao tulipanga kuwapeleka Sudan Kusini."

Azimio la Baraza la Usalama liliamua kuongeza askari 5,500 na polisi 440 na hivyo kufanya idadi ya kikosi kizima kufikia 12, 500.

Katika mashauriano hayo kuhusu Mwakilishi wa Katibu Mkuu kwenye Muungano wa Afrika Haile Menkerios alitoa ripoti kuhusu hali ya uhusiano kati ya Sudan na Sudan Kusini huku Hilde Johnson mwakilishi maalum wa Sudan Kusini akielezea hali ilivyo Sudan Kusini.