Ban awataka viongozi wa nchi za kati mwa Afrika kuzuia ukiukwaji wa haki za binadamu

9 Januari 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameyaambia mataifa ya ukanda wa kati mwa Afrika kuwa anasikitishwa sana na kuenea kwa ukiukwaji wa haki za binadamu katika eneo hilo, na kutaka mzunguko wa machafuko na ulipizaji kisasi miongoni mwa jamii vikomeshwe mara moja.

Bwana Ban amesema hayo katika ujumbe wake kwa mkutano wa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika ya Kati, ECCAS, ambao unafanyika mjini N’Djamena, Chad. . Ujumbe wa Bwana Ban umewasilishwa na Mwakilishi wake Maalumu ambaye pia ni Mkuu wa Ofisi ya Pamoja ya Kujenga Amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Babacar Gaye.

Katika ujumbe huo, Bwana Ban amesema inapaswa kwa pamoja kupeleka ujumbe kwa wale wote wanaotekeleza uhalifu na ukatili kuwa watawajibishwa kisheria, na kutoa wito wa kushirikiana ili kuzuia maafa zaidi na kuleta amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

Bwana Ban amesema, kwa mujibu wa Azimio la Baraza la Usalama namba 2127, Umoja wa Mataifa unaandaa kuweka tume ya kimataifa ya uchunguzi katika uhalifu na ukiukwaji wa haki za binadamu.