Bi. Kaag apatia Baraza la Usalama ripoti kuhusu Syria

8 Januari 2014

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo wakati wa mashauriano ya faragha, wamepatiwa taarifa kuhusu maendeleo ya uteketezaji wa mpango wa silaha za kemikali nchini Syria ikiwa ni siku moja baada ya ripoti ya kwamba shehena ya kwanza yenye vifaa vinavyohusiana na mpango huo imeondolewa nchini humo.

Taarifa hizo zimetolewa na Sigrid Kaag ambaye ni mratibu maalum wa jopo la pamoja la Umoja wa Mataifa na shirika la kimataifa la kupinga silaha za kemikali, OPCW na baada ya mashauriano hayo, Bi. Kaag alizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa hiyo ni hatua kubwa lakini bado changamoto ni kuendeleza kasi ya sasa.

(Sauti ya Bi. Kaag)

Tumezungumzia changamoto za usalama, mwelekeo wa badaye na baraza limeelezea matarajio ya pamoja kwamba kasi ya sasa iendelezwe,maendeleo yaonekane na kwamba ifikapo Juni mwaka huu wa 2014 kazi ya kuteketeza mpango wa silaha za kemikali Syria iwe imekamilika.”

China ni miongoni mwa nchi zinazotoa ulinzi kwa meli yenye shehena hiyo ambayo sasa imetia nanga eneo la kimataifa la baharini likisubiri shehena nyingine ambapo Mwakilishi wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Liu Jieyi amezungumzia maendeleo hayo mapya nchini Syria.

(Sauti ya Balozi Liu)

"Tunafurahi ya kwamba kwa ushirikiano na serikali ya Syria, tumeshuhudia maendeleo kwenye hilo, lakini bado hali ya usalama ni tete nchini humo, na bado hali ya usalama na mapigano vinatoa changamoto kubwa kwa kutokomeza silaha za kemikali. Tunatumai kuwa pande zote husika zitaweza mazingira stahili ili kuweza kuzinatia ratiba kwa mujibu wa azimio la baraza la usalama kuhusu utokomezaji wa mpango wa silaha za kemikali.”

Rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Januari Balozi Zaid Ra’ad Zedi Al Hassan akawajulisha waandishi wa habari walivyopokea ripoti hiyo.

(Sauti ya Balozi Al Hassan)

Wajumbe wamesifu hatua iliyofikiwa hadi sasa, lakini wametambua changamoto za utekelezaji wa kazi yao, ikiwemo vifaa na hata usalama kwa watendaji.”