UNHCR yaanza tena kuwasambazia misaada watu waliohamia uwanja wa ndege Bangui

8 Januari 2014

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, limeanza tena hapo jana kusambaza misaada ya kibinadamu kwa watu wapatao 100,000 walolazimika kuhama makwao, na ambao sasa wamepiga kambi kwenye uwanja wa ndege mjini Bangui, katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Shughuli ya ugawaji misaada ya kibinadamu ililazimika kuahirishwa mara kadhaa kwa sababu za kiusalama, na hivyo kutatiza uwezo wa kuwafikishia watu hao misaada.

Ugawaji wa pamoja wa chakula na vifaa vingine ulianza kufanywa mnamo Jumanne tarehe 7 Januari na UNHCR ikishirikiana na Shirika la Mpango wa Chakula, WFP. Hadi familia 20,000 kwenye uwanja huo wa ndege zinatarajiwa kupata misaada hiyo, ikiwemo mablanketi, mikeka ya kulalia, vyandarua vya kuzuia mbu, sabuni, mitungi ya maji na mifuko ya plastiki.