Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yahakikisha majeruhi Sudan Kusini wanapata tiba sahihi

WHO yahakikisha majeruhi Sudan Kusini wanapata tiba sahihi

Mapigano yanayoendelea nchiniSudan Kusini yamesababisha majeruhi zaidi ya 2,500 ambapo shirika la afya duniani, WHO na wadau wake linahakikisha wanapata matibabu sahihi pamoja na usaidizi wa vifaa tiba vinavyotakiwa.

WHO inasema inahakikisha majeruhi wanaohitaji tiba zaidi wanahamishiwa hospitali zenye uwezo ikiwemo ile yaJubaambako kuna madaktari bingwa wa upasuaji na hata wa tiba za kisaikolojia.

Miongoni mwao ni Dokta Kouassi Rene Kouame ambaye amesema usaidizi huo wa WHO umekuja wakati muafaka kwani bila hivyo wasingeweza kutoa usaidizi stahili akitolea mfano kuwa matibabu  yanahitaji dawa, na vifaa vinginevyo ikiwemo vya kufungia vidonda. Amesema bila msaada wa WHO wasingaliweza kutoa huduma hizo za matibabu.

Mmoja wa wagonjwa walionufaika na mpango huo, Kuol Fhar amesema ameweza kufanyiwa upasuaji wa mkono baada ya kujeruhiwa wakati wa mapigano makali huko Ayod, jimbo la Jonglei.

Wakati mapigano yakizidi kushamiri, Sudan Kusini, WHO inahakikisha imeweka mfumo wa kutambua mlipuko wa magonjwa haraka ili kuweza kuchukua hatua huku wakiratibu wabia wa afya kuhakikisha huduma zinafikia wanaohitaji zaidi.