Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kozi mpya katika haki za binadamu zaanzishwa vyuoni Kenya na Bolivia

Kozi mpya katika haki za binadamu zaanzishwa vyuoni Kenya na Bolivia

Kozi mpya za elimu kuhusu haki za binadamu zimeanzishwa katika Chuo Kikuu cha Laikipia nchini Kenya na Chuo cha Mafunzo ya Uongozi cha Bolivia kwa usaidizi wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Kozi hizo ambazo zitatolewa kwa wanafunzi wenye daraja ya shahada ya juu, yaani Master’s, zinalenga kuwapa wahudumu wa umma wa siku zijazo ujuzi, maadili na mitazamo ambayo itawapa msukumo kutetea haki zao wenyewe na haki za wengine.

Nchini Bolivia, wanafunzi watapata uelewa wa haki za binadamu katika muktadha wa kuzuia ubaguzi wa rangi, ambao umekita mizizi nchini humo dhidi ya jamii za asili na watu wenye asili ya Afrika.

Kozi ya haki za binadamu itatolewa kwa wanafunzi wote wa chuo kikuu cha Laikipia katika mwaka wa kwanza, ikizingatia viwango vya kimataifa na pia mfumo wa sheria nchini Kenya. Programu hii inatazamiwa kuanzishwa katika vyuo vingine vitano nchini Kenya ambavyo vimeiomba Ofisi ya Haki za Binadamu kuvisaidia.