China yateketeza tani 6.2 za meno ya tembo

6 Januari 2014

Biashara ya magendo ya meno ya tembo imekuwa na madhara makubwa kwa tembo wa Afrika, amesema Mtendaji Mkuu wa Mkataba wa kimataifa wa udhibiti wa biashara ya viumbe vilivyo hatarini kutoweka CITES, John Scalon huko Guangzhou, China hii leo wakati wa shughuli za kuteketeza tani Sita nukta Mbili za meno ya viumbe hao.

Bwana Scanlon amesema kitendo cha China kuteketeza mbele ya umma meno hayo yaliyokamatwa baada ya kuingizwa nchini humo kinyume cha sheria, ni ujumbe mzito kitaifa na kimataifa kuwa nchi hiyo haivumilii wala kukubali kabisa biashara hiyo haramu.

Mtendaji mkuu huyo wa CITES amesema ujumbe huo unapatiwa nguvu zaidi na ongezeko la idadi ya meno ya tembo yanayokamatwa, watu wanaofunguliwa mashtaka na kuhukumiwa nchini China kutokana na biashara hiyo haramu.

Amesifu jitihada za nchi mbali mbali ikiwemo za Afrika katika kukabiliana na biashara hiyo haramu akisema kuwa kupitia ubia huo dunia itaweza kubadili mwelekeo wa sasa wa ujangili wa tembo.

Takwimu za CITES zinaonyesha kuwa mwaka 2012 pekee tembo 22,000 waliuawa barani Afrika.