Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazungumzo kuhusu Sudan Kusini bado yakumbwa na mkwamo

Mazungumzo kuhusu Sudan Kusini bado yakumbwa na mkwamo

Idadi ya watu wanaokimbia Sudan Kusini kukwepa mapigano yanayoendelea kati ya vikosi vya serikali na wafuasi wa makamu wa rais wa zamani imeongezeka na kufikia Laki Moja na Elfu Themanini na Tisa huku baadhi yao wakisaka hifadhi nchi jirani. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya raia Elfu Ishirini na wawili wamesaka hifadhi nchi jirani ikiwemo Uganda huku wengine Elfu Sitini na mbili wakiwa wamejihifadhi kwenye ofisi za ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS. Umoja wa Mataifa kupitia mratibu wake wa usaidizi Toby Lanzer umesema mpango mpya wa kuwapatia wananchi hao maji, huduma za afya, malazi na chakula utatekelezwa kwa miezi ya Januari, Februari na Machi. Hata hivyo anasema suala la usalama bado ni changamoto kusafirisha misaada.

(Sauti ya Toby Lanzer)

"Ni hatari sana wakati huu kusafiri kwa kutumia karibu barabara zote. Kwa sasa tunategemea zaidi usafirishaji kwa anga ambao ni mgumu kwa upande wa gharama. Kusafirisha vyakula kwa ndege mara nyingi ina ugumu wake lakini tunafanya hakuna njia nyingine.”

Wakati hayo yakijiri mazungumzo yenye lengo la kusitisha mapigano kati ya pande mbili husika ambayo yalianza mwanzoni mwaka huu huko Addis Ababa Ethiopia hayajazaa matunda yoyote.

Wakati huo huo, raia wa kigeni 1,500 waliokuwa wamesaka hifadhi kwenye ofisi za UNMISS huko Bentiu jimbo la Unity, wamehamishiwa Juba au mji wa Heglig nchini Sudan. Afisa wa masuala ya kiraia ndani ya UNMISS Katia da Silva amesema wengi wao wamepoteza mali zao, wamekumbwa na vipigo na hata kubakwa. Idadi kubwa ya raia hao wanatoka Eritrea, Ethiopia, Kenya, Uganda, Sudan, Rwanda, DR Congo, Burundi, Chad, India, Ufipilipino, Marekani, Canada na Australia.