Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wajiandaa kwa mkutano wa ahadi za kuisaidia Syria

UM wajiandaa kwa mkutano wa ahadi za kuisaidia Syria

Umoja wa Mataifa umesema unajitahidi kuhakikisha kwamba mkutano wa ahadi za usaidizi kwa Syria uliopangwa kufanyika Kuwait katikati ya Januari unakuwa wa mafanikio. Mkutano huo una lengo la kukusanya msaada wa fedha wa kimataifa ili kukidhi mahitaji ya lazima ya kibinadamu kwa raia wa Syria zaidi ya milioni 9, wakati huu machafuko yakiendelea nchini mwao. Valarie Amos , mkuu wa shirika la Umoja wa mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA amesema kadri siku zinavyokwenda hali inazidi kuzorota Syria.

Amesema na watu wa misaada wana kiwango cha kusaidia , wanajitahidi kuwasaidia watoto, wanawake na wanaume walioathirika na vita vilivyosababisha maafa makubwa. Bi Amos ameongeza kuwa msaada unaohitajika ni wa muhimu saana na tarehe 15 mwezi huu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ataongoza mkutano wa ahadi kwa ajili ya watu wa Syria utakaoandaliwa na Kuwait.
Ameongeza kuwa katikati ya Desemba mwaka jana Umoja wa mataifa ulitoa ombi la dola bilioni 6.5 ili kuwasaidia Wasyria kwa mwaka huu ambalo lilikuwa ombi kubwa kabisa kuwahi kutolewa kwa janga moja la kibinadamu. Umoja wa mataifa unakadiria kuwa Wasyria milioni 6.5 wamekuwa wakimbizi wa ndani na wengine zaidi ya milioni 2.2 wametafuta ukimbizi katika nchi jirani za Lebanon, Jordan, Uturuki, Iraq na Misri.