Hatua zichukuliwe kukomesha ghasia dhidi ya waandishi Iraq:UNESCO

3 Januari 2014
Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO Bi Irina Bokova, Ijumaa ameelezea hofu yake baada ya mauaji ya wafanyakazi sita wa vyombo vya habari hivi karibuni katika matukio mawili tofauti nchini Iraq.
Amesema analaani vikali mauaji ya Raad Yassin, Jamal Abdel Nasser, Mohamed Ahmad Al-Khatib, Wissam Al-Azzawi na Mohamed Abdel Hamid katika shambulio kwenye televisheni ya Salaheddin TV mjini Tikrit, na mauaji ya fOmar Al-Dulaimy kwenye mji wa Ramadi.
Bi Bokova ameutaka uongozi wa Iraq kufanya kila liwezekanalo kuwafikisha mbele ya sheria wahusika kujimu mashitaka ya uhalifu hu. Amesema ongezeko la ghasia dhidi ya vyombo vya habari nchini Iraq halivumiliki kwani ni tishio kubwa kwa maridhiano ya kitaifa na ujenzi mpya wa taifa hilo.
Omar Al-Dulaimy aliuawa tarehe 31 Desemba alipokuwa akiripoti kuhusu mapigano mjini Ramadi alipokuwa mwandishi wa Radio Ramadi huku wafanyakazi watano wa Salaheddin TV waliuawa katika shambulio la kujitoa muhanga kwenye makao makuu ya televisheni yao mjini Tikrit Desemba 23 mwaka jana.