IOM yatenga fungu kusaidia kusafirisha wahamiaji CAR:

3 Januari 2014

Mkurugenzi mkuu wa shirika la kimataifa la uhamiaji IOM bwana William Lacy Swing wiki hii ameidhinisha fungu la dharura la fedha kwa ajili ya kuanza kuwasafirisha kwa ndege wahamiaji walioathirika na mapigano yanayoendelea nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR). Amesema IOM imepokea maombi kutoka katika serikali nyingi ya kutaka raia wao wasafirishwe kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati. 

Bwana Swingi ameongeza kuwa fedha alizoidhinisha ni dola 200,000 ili kuanza operesheni hiyop kwani ni lazima kuwasaidia wahamiaji waliokwama CAR ambao maisha yao yamo hatarini  Wahamiaji nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati wanakadiriwa kuwa ni maelfu kwa maelfu wengi wakitokea nchi jirani zikiwemo Cameroon, Chad, Ivory Coast, Niger, Nigeria na Sudan.

Serikali ya Niger inakadiria kwamba raia wake 900 wanahitaji msaada wa haraka nchini CAR, Sudan ina rai wapatao 275, Mali 500 wanaotaka kusaidia,na Chad zaidi ya raia wake 100,000 wanasemakana kusalia Jamhuri ya Afrika ya Kati  wakati wengine 12,000 wamerejea nyumbani tangu tarehe Mosi Januari 2014.