Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yataka wasirejeshwe Bulgaria waomba hifadhi

UNHCR yataka wasirejeshwe Bulgaria waomba hifadhi

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR Ijumaa limetoa tamko la kuyataka mataifa yanayoshiriki katika sheria Dublini kusitisha hatua ya kuwasafirisha waomba hifadhi kurejea Bulgaria. Joseph Msami na habari kamili

(TAARIFA YA JOSEPH MSAMI)
UNHCR imesema waomba hifadhi nchini Bulgaria wanakabiliwa na hatari ya vitendo visivyo vya kibinadamu au kudhalilishwa kutokana na mapungufu yaliyopo katika mfumo mzima unaohusika na hali ya mapokezi na taratibu za kusajili waomba hifadhi. 
Tathimini ya shirika hilo inaonyesha kwamba waomba hifadhi nchini Bulgaria kila wakati wanakosa huduma muhimu kama chakula na afya, wanachukua muda mrefu kusajiliwa hali ambayo inawakosesha haki zao za mshingi na wanakuwa katika hatari ya kuwekwa rumande.
Zaidi ya hayo UNHCR inasema kuna changamoto kubwa za kutathimini kwa haki taratibu za usajili wa waomba hifadhi na pia ripoti za wengi kurejeshewa mpakani. Sheria za Dublin zinatoa fursa ya mfumo wa kuwajibika kwa kuchunguza madai ya kuomba hifadhi yaliyowasilishwa katika nchi wanachama wa Muungano wa Ulaya na mengine yaliyo sehemu ya sheria za Dublin kwa kuzingatia vigezo maalumu.
UNHCR inasema lengo ni kuhakikisha kila dai linapewa uzito sawia na nchi hizo kwa kushughulikia maombi mengi zaidi na kwa njia inayostahili. Imeongeza kuwa licha ya hatua kubwa zilizopigwa bado kuna pengo katika utekelezaji wa sheria na sera za kimataifa za kulinda waomba hifadhi nchini Bulgaria.